Nafahamu kwamba katika maisha ya kila siku hayakosekani mambo ya kuumiza. Sina
shaka kuugua, kufiwa, kukosa chakula, kusalitiwa katika mapenzi, kudhurumiwa,
kufilisika na kufutwa kazi ni mambo ambayo huzaa huzuni na machozi miongoni mwa
watu wengi. Lakini jambo la kujiuliza ni kwamba unalia au kuhuzunika kwa
sababu matatizo yako ni makubwa au umekosa kufahamu kanuni ya maisha aliyoitoa Mungu.Hebu jiulize ni wangapi wanahuzunikia mishahara midogo wanayolipwa makazini mwao, Je katika huzuni hizo ulishawahi kuwaza kwamba kuna binadamu
wengine hawana kazi na wanahangaika kutafuta shilingi mia tano kwa kuuza mihogo
na karanga kwenye kona za mitaa huku wakiwa juani?. Kama hao wapo ukubwa wa
tatizo la kukosa kazi unaokuliza kila siku uko wapi?
Uko wapi ukubwa wa tatizo la kutokuzaa
wakati kuna waliozaa na watoto wote wakafa. Kimsingi uwiano wa shida na
uhimili wake unaopatikana baina ya mtu na mtu, kamwe sifa ya huzuni hailetwi na
ukubwa wa tatizo, isipokuwa ni kukosekana kwa sanaa ya kuishi, yenye maono na
hisia za kupunguza mambo makubwa kuwa madogo.Katika hisia, mwanadamu hawezi
kuzuia machozi ya furaha au huzuni yasitoke, maana nilisoma katika Biblia kuwa
hata Yesu alilia pale alipopata habari kwamba rafiki yake Lazaro amekufa.
Lakini pamoja na kilio hicho hakusita kuita maono na kuona kwamba tatizo
lililokuwa mbele yake lilikuwa dogo, akaamua kuchukua hatua ya kuwaagiza
wanakijijini waliondoe jiwe na yeye kutajwa kumfufua kwa kutumia uwezo wake
(Haya ni ya kidini siyajadili sana katika mada hii).
Ifahamike kwamba kila mwanadamu ana uwezo wake wa kufanya, zaidi ya tatizo
analokutana nalo, lakini uwezo huo hauji kama sanaa ya maono na ‘udogoshaji’
matatizo haujapewa kipaumbele. Kuna watu wanalia kila siku kwa kuhitaji utajiri, lakini hawafikii
malengo kwa sababu wanaona umasikini ni jambo kubwa na kuufikia utajiri ni
jambo kubwa pia.Kwa mujibu wa utafiti wa William Frey mkemia na Mkurugenzi
wa Kituo cha Dry Eye and Tear Reseach cha Minneapolis, watu hulia katika
makundi matano tofauti ambayo ni: Wenye kujawa na huzuni zinazosababishwa na
matatizo ya kimaisha 49%.Wanaolia kwa furaha ni alisilimia 21, hasira 10% na
huruma 7%, huku wenye wasiwasi wakilia kwa kiwango cha asilimi 5 juu ya wenye
hofu wanaolia kwa asilimia 4.Lakini, pamoja na kuwepo kwa makundi hayo sita,
mwanadamu mwenyewe anatajwa kuwa na uwezo wa kuyabadili maono yake kwa kila
kundi na kupata matokeo tofauti kabisa, kwani hasira ikipunguzwa kwa kuona
kichocheo kilichojaza hasira ni kidogo pumzi hushuka na mtu hujiona mwenye
utulivu tofauti na mwanzo.
Vivyo hivyo, kwa anayelia kwa huzuni, huruma, wasiwasi na hofu,Kwa mantiki ile
ile hakuna haja ya kuhuzunika kwa kiwango cha juu, wakati kuna kiwango cha
chini cha kujiweka huru, nacho ni cha kutazama mambo makubwa kama madogo yasiyodumu na kwamba
saa, siku, miaka michache ijayo yatapita. Jiulize hapo ulipo msomaji wangu ni
kitu gani kinakuliza? Fahamu kwamba hulii au kuhuzunika kwa sababu matatizo ni
makubwa, bali umekosa ufahamu wa maono.Hebu chukua jukumu la kudharau shida
zako kwa kujilinganisha na wengine ambao bila shaka wanakuzidi matatizo. Fanya
hivyo kila unapokabiliwa na tatizo, usilione tatizo ni kubwa kwa takwimu,
lichukulie kuwa ni dogo kisha uanze kulishughulikia, utaona linamalizika kwa
ushindi mkubwa. Kamwe usijaribu kulitatua ndani ya maono yanayolikuza, hutapata
matokeo mazuri.Ukiwa ni umasikini uone ni mdogo, kututokuzaa, kukosa kazi,
kuteswa na mume na matatizo yote yatakayokukuta katika maisha yako yaone ni
madogo kisha tumia nguvu zako zote kuyakabili nina hakika utayashinda kirahisi.
Jaribu kupunguza matatizo, badala ya
kuyakuza kwa kuona hayawezekani kutatuliwa, utaona maajabu. Tambua kuwa tatizo lako si kubwa
bali unalikuza katika mawazo yako, kwa kuwa wapo wenye matatizo makubwa zaidi yao na hawalii
kama wewe.
No comments:
Post a Comment