Tuesday, November 27, 2012

KWA NINI KUACHANA?



Matatizo yanayochangia watu kuachana yako mengi, ambayo mtu unaweza kujaza vitabu kuyaelezea, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi huachana kutokana na udhaifu wa sababu zilizowasababisha kupendana. Kwa mfano wapenzi ambao wakati wa kupendana kwao walitamaniana kwa maumbo, sura, mvuto wa kingono na pesa huwa katika hatari ya kuachana baada ya vitu vilivyowasukuma kupendana kupoteza mvuto.

Hakuna asiyefahamu kuwa watu hubadilika tabia, umbo, sura, hufirisika na hata kutovutia tena! Hivyo mtu anapopenda kwa sababu hizo, ukomo wake huwa ni baada ya alichopenda kuondoka. Ukipenda kwa tamaa ya ngono ukishashibishwa nayo hutakuwa na sababu ya kumpenda mpenzi wako, matokeo yake utamwacha.Ukiwa umeamua kumpenda dada fulani kwa sababu anavutia, kumbuka kuwa anaweza kupata ajali akapoteza mvuto au akazeeka. Je umeshajiuliza swali itakuwaje kama mpenzi wako atapata makovu, utafanyaje baada ya mvuto wake wa usichana kuisha, nini kitafuata baada huyo mwanaume unayemsifia kwa tendo la ndoa atakapofikia ukomo wa kukutosheleza? Nadhani ni kuachana.

Sababu nyingine inayochangia wapenzi kuachana ni kutojali changuo sahihi kulingana na jinsi mtu mwenyewe alivyo.Mimi niliwahi kusoma katika Biblia Mungu akiweka wazi namna alivyozingatia kumuumbia mke Adamu kwa kusema, alimuumba mtu wa kufanana naye. Hivyo ni busara kupata mpenzi wa kufanana na wewe kwa tabia na mambo mengine ya msingi, bila hivyo mapenzi hayawezi kudumu.Kwa mfano kama wewe ni mtu wa imani kali, inakuwaje unakwenda kupendana na mpagani, huoni hicho kitakuwa kikwazo cha penzi lenu? Kwa msingi huo, lazima kupendana kuambatane na kufanana elimu, mtazamo na hata tamaduni, hii itasaidia kuondoa vikwazo vya mapenzi kuvunjika.

Lakini jambo jingine linalowafanya wapenzi wengi kuachana ni kutojali au kutofahamu kanuni za kutunza penzi. Kuna watu wanaweza kuchaguana kwa kuzingatia maelekezo yote, lakini wakajikuta wanaachana kwa kutojua namna ya kukuza na kudumisha upendo wao.

Nasema hivyo kwa sababu, kumpata mpenzi ni jambo jingine na kumtunza ni hatua nyingine ambayo ni ya msingi. Inawezekana kabisa ukampata wa kufanana naye, lakini ukajikuta unashindwa kudumu naye kwa sababu ya kumuudhi mara kwa mara tena kwa kusudi, kumnyanyasa, kusikiliza umbea, wivu, kutomjali na kumpuuza.Kinachosikitisha sana katika mapenzi ni kuona watu wanawapata wapenzi wa kweli, badala ya kufurahika nao wanawachezea kwa kufanya vurugu na kuwa waanzilishi wa usaliti na ujeuri. Ushauri wangu ni kuwa, ukipata wa kukupenda usimchezee, mtunze na umuonyeshe kweli kuwa wewe ni wa kufanana naye.

Mwisho, mapenzi lazima yakose sababu, ukiulizwa unampendea nini mpenzi wako? Jibu liwe sijui, kwani ukitaja sababu yoyote unakuwa katika hatari ya kuachana kwa vile kila sababu ina mwisho wake. Penzi ni lidhiko la moyo lisilokuwa na kwa nini. Ukisema nampenda kwa sababu ananijali, asipokujali, ukisema ni mzuri akiwa mbaya, ana pesa akiishiwa, mtundu,..uwanjani akichoka? Bila shaka penzi nalo litachoka!

Makaya's Forum: AMUA YAKO.

Makaya's Forum: AMUA YAKO.: Duniani wengi humkimbia mtu kipindi cha kifo,maana wakiona taabu ndiyo utasikia Yule kachanganyikiwa kabisa,akiamini kufika darasani ...

ONA MATATIZO YAKO MADOGO.


Nafahamu kwamba katika maisha ya kila siku hayakosekani mambo ya kuumiza. Sina shaka kuugua, kufiwa, kukosa chakula, kusalitiwa katika mapenzi, kudhurumiwa, kufilisika na kufutwa kazi ni mambo ambayo huzaa huzuni na machozi miongoni mwa watu wengi. Lakini jambo la kujiuliza ni kwamba unalia au kuhuzunika kwa sababu matatizo yako ni makubwa au umekosa kufahamu kanuni ya maisha aliyoitoa Mungu.Hebu jiulize ni wangapi wanahuzunikia mishahara midogo wanayolipwa makazini mwao, Je katika huzuni hizo ulishawahi kuwaza kwamba kuna binadamu wengine hawana kazi na wanahangaika kutafuta shilingi mia tano kwa kuuza mihogo na karanga kwenye kona za mitaa huku wakiwa juani?. Kama hao wapo ukubwa wa tatizo la kukosa kazi unaokuliza kila siku uko wapi?

Uko wapi ukubwa wa tatizo la kutokuzaa wakati kuna waliozaa na watoto wote wakafa. Kimsingi uwiano wa shida na uhimili wake unaopatikana baina ya mtu na mtu, kamwe sifa ya huzuni hailetwi na ukubwa wa tatizo, isipokuwa ni kukosekana kwa sanaa ya kuishi, yenye maono na hisia za kupunguza mambo makubwa kuwa madogo.Katika hisia, mwanadamu hawezi kuzuia machozi ya furaha au huzuni yasitoke, maana nilisoma katika Biblia kuwa hata Yesu alilia pale alipopata habari kwamba rafiki yake Lazaro amekufa. Lakini pamoja na kilio hicho hakusita kuita maono na kuona kwamba tatizo lililokuwa mbele yake lilikuwa dogo, akaamua kuchukua hatua ya kuwaagiza wanakijijini waliondoe jiwe na yeye kutajwa kumfufua kwa kutumia uwezo wake (Haya ni ya kidini siyajadili sana katika mada hii).

Ifahamike kwamba kila mwanadamu ana uwezo wake wa kufanya, zaidi ya tatizo analokutana nalo, lakini uwezo huo hauji kama sanaa ya maono na ‘udogoshaji’ matatizo haujapewa kipaumbele. Kuna watu wanalia kila siku kwa kuhitaji utajiri, lakini hawafikii malengo kwa sababu wanaona umasikini ni jambo kubwa na kuufikia utajiri ni jambo kubwa pia.Kwa mujibu wa utafiti wa William Frey mkemia na Mkurugenzi wa Kituo cha Dry Eye and Tear Reseach cha Minneapolis, watu hulia katika makundi matano tofauti ambayo ni: Wenye kujawa na huzuni zinazosababishwa na matatizo ya kimaisha 49%.Wanaolia kwa furaha ni alisilimia 21, hasira 10% na huruma 7%, huku wenye wasiwasi wakilia kwa kiwango cha asilimi 5 juu ya wenye hofu wanaolia kwa asilimia 4.Lakini, pamoja na kuwepo kwa makundi hayo sita, mwanadamu mwenyewe anatajwa kuwa na uwezo wa kuyabadili maono yake kwa kila kundi na kupata matokeo tofauti kabisa, kwani hasira ikipunguzwa kwa kuona kichocheo kilichojaza hasira ni kidogo pumzi hushuka na mtu hujiona mwenye utulivu tofauti na mwanzo.

Vivyo hivyo, kwa anayelia kwa huzuni, huruma, wasiwasi na hofu,Kwa mantiki ile ile hakuna haja ya kuhuzunika kwa kiwango cha juu, wakati kuna kiwango cha chini cha kujiweka huru, nacho ni cha kutazama mambo makubwa kama madogo yasiyodumu na kwamba saa, siku, miaka michache ijayo yatapita. Jiulize hapo ulipo msomaji wangu ni kitu gani kinakuliza? Fahamu kwamba hulii au kuhuzunika kwa sababu matatizo ni makubwa, bali umekosa ufahamu wa maono.Hebu chukua jukumu la kudharau shida zako kwa kujilinganisha na wengine ambao bila shaka wanakuzidi matatizo. Fanya hivyo kila unapokabiliwa na tatizo, usilione tatizo ni kubwa kwa takwimu, lichukulie kuwa ni dogo kisha uanze kulishughulikia, utaona linamalizika kwa ushindi mkubwa. Kamwe usijaribu kulitatua ndani ya maono yanayolikuza, hutapata matokeo mazuri.Ukiwa ni umasikini uone ni mdogo, kututokuzaa, kukosa kazi, kuteswa na mume na matatizo yote yatakayokukuta katika maisha yako yaone ni madogo kisha tumia nguvu zako zote kuyakabili nina hakika utayashinda kirahisi.

Jaribu kupunguza matatizo, badala ya kuyakuza kwa kuona hayawezekani kutatuliwa, utaona maajabu. Tambua kuwa tatizo lako si kubwa bali unalikuza katika mawazo yako, kwa kuwa wapo wenye matatizo makubwa zaidi yao na hawalii kama wewe.

Makaya's Forum: ELEWA 2

Makaya's Forum: ELEWA 2 :   Mateso ya moyo huudhoofisha undani wa mwili,unaweza kubadili mwelekeo hata ule uliotakiwa kuelekea baadaye n...