Tuesday, November 27, 2012

ONA MATATIZO YAKO MADOGO.


Nafahamu kwamba katika maisha ya kila siku hayakosekani mambo ya kuumiza. Sina shaka kuugua, kufiwa, kukosa chakula, kusalitiwa katika mapenzi, kudhurumiwa, kufilisika na kufutwa kazi ni mambo ambayo huzaa huzuni na machozi miongoni mwa watu wengi. Lakini jambo la kujiuliza ni kwamba unalia au kuhuzunika kwa sababu matatizo yako ni makubwa au umekosa kufahamu kanuni ya maisha aliyoitoa Mungu.Hebu jiulize ni wangapi wanahuzunikia mishahara midogo wanayolipwa makazini mwao, Je katika huzuni hizo ulishawahi kuwaza kwamba kuna binadamu wengine hawana kazi na wanahangaika kutafuta shilingi mia tano kwa kuuza mihogo na karanga kwenye kona za mitaa huku wakiwa juani?. Kama hao wapo ukubwa wa tatizo la kukosa kazi unaokuliza kila siku uko wapi?

Uko wapi ukubwa wa tatizo la kutokuzaa wakati kuna waliozaa na watoto wote wakafa. Kimsingi uwiano wa shida na uhimili wake unaopatikana baina ya mtu na mtu, kamwe sifa ya huzuni hailetwi na ukubwa wa tatizo, isipokuwa ni kukosekana kwa sanaa ya kuishi, yenye maono na hisia za kupunguza mambo makubwa kuwa madogo.Katika hisia, mwanadamu hawezi kuzuia machozi ya furaha au huzuni yasitoke, maana nilisoma katika Biblia kuwa hata Yesu alilia pale alipopata habari kwamba rafiki yake Lazaro amekufa. Lakini pamoja na kilio hicho hakusita kuita maono na kuona kwamba tatizo lililokuwa mbele yake lilikuwa dogo, akaamua kuchukua hatua ya kuwaagiza wanakijijini waliondoe jiwe na yeye kutajwa kumfufua kwa kutumia uwezo wake (Haya ni ya kidini siyajadili sana katika mada hii).

Ifahamike kwamba kila mwanadamu ana uwezo wake wa kufanya, zaidi ya tatizo analokutana nalo, lakini uwezo huo hauji kama sanaa ya maono na ‘udogoshaji’ matatizo haujapewa kipaumbele. Kuna watu wanalia kila siku kwa kuhitaji utajiri, lakini hawafikii malengo kwa sababu wanaona umasikini ni jambo kubwa na kuufikia utajiri ni jambo kubwa pia.Kwa mujibu wa utafiti wa William Frey mkemia na Mkurugenzi wa Kituo cha Dry Eye and Tear Reseach cha Minneapolis, watu hulia katika makundi matano tofauti ambayo ni: Wenye kujawa na huzuni zinazosababishwa na matatizo ya kimaisha 49%.Wanaolia kwa furaha ni alisilimia 21, hasira 10% na huruma 7%, huku wenye wasiwasi wakilia kwa kiwango cha asilimi 5 juu ya wenye hofu wanaolia kwa asilimia 4.Lakini, pamoja na kuwepo kwa makundi hayo sita, mwanadamu mwenyewe anatajwa kuwa na uwezo wa kuyabadili maono yake kwa kila kundi na kupata matokeo tofauti kabisa, kwani hasira ikipunguzwa kwa kuona kichocheo kilichojaza hasira ni kidogo pumzi hushuka na mtu hujiona mwenye utulivu tofauti na mwanzo.

Vivyo hivyo, kwa anayelia kwa huzuni, huruma, wasiwasi na hofu,Kwa mantiki ile ile hakuna haja ya kuhuzunika kwa kiwango cha juu, wakati kuna kiwango cha chini cha kujiweka huru, nacho ni cha kutazama mambo makubwa kama madogo yasiyodumu na kwamba saa, siku, miaka michache ijayo yatapita. Jiulize hapo ulipo msomaji wangu ni kitu gani kinakuliza? Fahamu kwamba hulii au kuhuzunika kwa sababu matatizo ni makubwa, bali umekosa ufahamu wa maono.Hebu chukua jukumu la kudharau shida zako kwa kujilinganisha na wengine ambao bila shaka wanakuzidi matatizo. Fanya hivyo kila unapokabiliwa na tatizo, usilione tatizo ni kubwa kwa takwimu, lichukulie kuwa ni dogo kisha uanze kulishughulikia, utaona linamalizika kwa ushindi mkubwa. Kamwe usijaribu kulitatua ndani ya maono yanayolikuza, hutapata matokeo mazuri.Ukiwa ni umasikini uone ni mdogo, kututokuzaa, kukosa kazi, kuteswa na mume na matatizo yote yatakayokukuta katika maisha yako yaone ni madogo kisha tumia nguvu zako zote kuyakabili nina hakika utayashinda kirahisi.

Jaribu kupunguza matatizo, badala ya kuyakuza kwa kuona hayawezekani kutatuliwa, utaona maajabu. Tambua kuwa tatizo lako si kubwa bali unalikuza katika mawazo yako, kwa kuwa wapo wenye matatizo makubwa zaidi yao na hawalii kama wewe.

No comments:

Makaya's Forum: ELEWA 2

Makaya's Forum: ELEWA 2 :   Mateso ya moyo huudhoofisha undani wa mwili,unaweza kubadili mwelekeo hata ule uliotakiwa kuelekea baadaye n...